AfyaMtandao

Madhehebu ya dini yaanzisha Jukwaa la majadiliano kupambana na Ukimwi

Madhehebu ya dini ya Wakristo na Waislamu yamesaini makubaliano ya kuanzisha jukwaa la pamoja la majadiliano kuona namna gani watakavyoweza  kupambana na  maambukizi ya ugonjwa wa Ukimwi kwa waumini wao.

Jukwaa hilo linalofahamika kama “Tanzania AIDS Interfaith Forum” (TAIFO) litaratibu na kusimamia shughuli za pamoja za kuzuia maambukizi  ya  Ukimwi kwa kutoa huduma itakayoboresha afya za watu wanaoishi na Virus vya Ukimwi na kutoa msukumo katika kubadili tabia kwa jamii, hasa katika kuwajengea uwezo, na kuwa na mijadala ya pamoja ya kushirikishana taarifa ya namna gani pande zote mbili hizo zinavyojihusisha katika kupambana na Ukimwi  na zinavyowashirikisha waumini wao kwa lengo la kuboresha maisha ya watanzania wote.

Makubaliano hayo ambayo yamesainiwa baina ya Tume ya Kikristo ya huduma za jamii “Christian Social Services Commission” (CSSC) kwa niaba ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Baraza la Kikristu Tanzania (CCT) and Baraza la Makanisa ya Pentekoste Tanzania (PCT) na Mtandao wa Waislamu Tanzania “Tanzania Muslim Welfare Network (TMWN) Kwa niaba ya jumuia kadhaa za kiislam, yameratibiwa na kufanikishwa na Tume ya Taifa ya kudhibiti Ukimwi (TACAIDS), na  yamelenga kuwahusisha kwa karibu viongozi wa dini kuwaeleza kwa uwazi waumini wao umuhimu wa kuepuka maambukizi ya Ukimwi.

Akizungumza wakati wa utianaji saini makubalino hayo uliyofanyika mjini Morogoro, Mwenyekiti mtendaji wa Tume ya Taifa ya Kudhibiti Ukimwi, (TACAIDS) Dk. Fatuma  Hassan  Mrisho  amesema, madhehebu ya dini kupitia viongozi wao yana nafasi kubwa ya kuwaelimisha waumuni wao jinsi ya kuepuka maambukizi ya Ukimwi kwa kufuata misingi na maadili ya dini zao kama zinavyowataka, kwani dini zote zinapinga zinaa. Amewaomba wawe daraja la kuwataka waumini wao kubadili tabia.

Dk. Fatuma amesema kulingana na utafiti uliofanywa na Shirika la utafiti la Lake Victoria Nile Basin, umebaini kuwa maeneo ya visiwani maambukizi ni makubwa, asilimia 20 hadi 25. Amewaomba viongozi wa dini kutambua meneo ya vichocheo na kuweka nguvu zaidi pale ambapo kuna maambukizi makubwa. Ametoa mfano kuwa nchi ya Uganda ilikuwa na maambukizi makubwa  asilimia 18 lakini sasa yamepungua sana kwa zaidi ya asilimia 48, na hali ya kupungua huko imetokana na  kuwashirikisha viongozi wa dini ambao kauli na nguvu zao ni kubwa kwa waumini wao.

Aidha Dk. Fatuma, amesisitiza suala la jinsia lipewe kipau mbele na wanawake wasitengwe washirikishwe katika hatua zote za kupambana na Ukimwi.

Naye Mwenyekiti wa Mtandao wa waislamu  Tanzania (TMWN), Sheikh Issa Othman Issa akiongea kwa niaba ya mtandao huo amesema, Jukwaa hilo ni muhimu sana kuwaleta pamoja waislimu  na wakristo kuangalia namna gani wataweza kupambana na tatizo la ugonjwa wa Ukimwi ambalo linazidi kukua kadri siku zinavyokwenda. Amelitaka jukwaa hili kuwa muhimili mkubwa wa kuwaelimsha waumini wao kujikinga na maambukizi mapya ya Ukimwi kwa wale ambao tayari wana maambukizi na hata wale ambao bado hawajaambukizwa kujikinga.

Naye katibu mkuu wa umoja wa makanisa ya pentekoste (PCT) Mhashamu askofu Mwasota, akishukuru kwa niaba ya CSSC, ameziomba pande zote mbili hizo kuhakikisha kuwa maazimio ya kuanzisha chombo hicho yanatekelezwa kama jinsi walivyokubaliana.

 

Views: 398

Add a Comment

You need to be a member of AfyaMtandao to add comments!

Join AfyaMtandao

© 2024   Created by sona.   Powered by

Badges  |  Report an Issue  |  Terms of Service