AfyaMtandao

Halmashauri ya wilaya ya Rufiji yapewa vifaa kuboresha Huduma ya mama na mtoto

Mradi wa kuboresha Huduma ya akina mama na watoto kwa njia ya TEHAMA “e-RCH for Better Care” unaotekelezwa kwa pamoja kati ya Tume ya Kikristu ya Huduma za jamii (CSSC), kupitia mradi wa AfyaMtandao, Chuo kikuu cha Afya Muhimbili kupitia kitengo cha elimu kwa njia ya mtandao, Shirika la ITIDO sambamba na Kampuni ya SoftMed, umetoa Kompyuta 2 na simu za mikononi 42 ambazo zitatumika katika shughuli za mradi kukusanya na kuhifadhi taarifa za akina mama wajawazito na watoto walio chini ya miaka 5.

Akikabidhi vifaa hivyo mwakilishi wa mradi huo Bw. Twaha Mubaraka, amesema vifaa hivyo ni mali ya halmashauri na mradi unatarajia kuona kuwa vinatumika kwa kazi iliyokusudiwa katika kukusanya na kuhifadhi taarifa za wahuska.

Akielezea kuhusu Simu hizo Bw. Twaha amebainisha kuwa simu hizo zimefungwa mfumo maalumu ambao utatumika katika kuweka taarifa sahihi za akina mama wajawazito na watoto kutoka maeneo mbalimbali ya wilaya ya Rufiji na taarifa hizo zitakuwa zikipokelewa na hospitali ya wilaya Utete na Mchukwi ambazo zitafungwa Kompyuta na kutumika kutunza taarifa hizo.

Mfumo huo utarahisisha tathimini ya takwimu sahihi ambazo zitafanyiwa kazi katika kutoa maamuzi ya kuboresha huduma za afya kwa upande wa akina mama na watoto wilayani humo. Lakini pia simu hizo kupitia mfumo huo zinawezesha daktari aliyeko hospitali ya wilaya Utete au Mchukwi kuona vidokezo vya hatari kwa mama mjamzito ambaye taarifa zake tayari zimewekwa katika mfumo huo, hivyo kutoa nafasi kwa daktari mhusika kufuatilia maendeleo ya mama huyo na kuhimiza kuhudhuria Kliniki. Pia simu hizo zitatumika katika Huduma ya rufaa pamoja na ushauri katika mfumo wa Tibamtandao ambapo madaktari bingwa kadhaa watakuwa wameunganishwa katika mfumo huo.

Akipokea vifaa hivyo, Mganga mkuu wa wilaya ya Rufiji Dk. Fakii Mohamed Kombo, ameshukuru mradi huo kwa kutoa vifaa hivyo na kusema kuwa simu hizo zitatumiwa na waganga sambamba na watoa Huduma za afya kwa jamii (CHW) waliopo katika vijiji mbalimbali vya wilaya hiyo. Aidha Dk. Kombo amesema kuwa simu hizo ni nyenzo bora katika kufanikisha lengo hilo la kusaidia kuokoa maisha ya mama na mtoto.Vifaa hivyo vimegharimu pesa za Kitanzania kiasi cha shilingi milioni sita na nusu.

Wilaya ya Rufiji ni moja ya wilaya ambazo zinakabiliwa na changamoto za kina mama wengi kushindwa kujifungulia hospitali ambapo inakadiriwa kuwa miongoni mwa akina mama wajawazito wanaohudhulia Kliniki zaidi ya asilimia 50 wanajifungulia nyumbani, huku  ikielezwa kuwa sababu ni kutokana na umbali wa vituo vya kutolea Huduma za afya.

Mradi wa “e-RCH for Better Care” unafadhiliwa na Shirika la Spider kupitia idara ya Kompyuta ya Chuo Kikuu cha Stockholm Sweden.

Views: 224

Add a Comment

You need to be a member of AfyaMtandao to add comments!

Join AfyaMtandao

© 2024   Created by sona.   Powered by

Badges  |  Report an Issue  |  Terms of Service