AfyaMtandao

Mfumo wa Kompyuta wa AfyaPro kufungwa hospitali ya Sengerema

Hospitali teule ya wilaya ya Sengerema inayomilikiwa na Kanisa Katoliki Jimbo la Geita iko mbioni kuanza kutumia mfumo wa “AfyaPro” wa kukusanya na kuhifadhi  taarifa za afya kwa njia ya Kompyuta. Imeelezwa kuwa mfumo huo utafungwa katika idara tatu ambazo ni; mapokezi kwa ajili ya wagonjwa wa ndani na nje, maabara na katika kitengo cha upasuaji.

Meneja wa mradi wa “D-HMIS” ambao unaratibu ufungaji wa mfumo huo Bw. Deogratias Katonyela anasema, maandalizi ya ufungaji wa mfumo huo yanaendelea vizuri, ambapo uunganishaji wa maeneo husika unafanyika na mafunzo ya awali tayari yamefanyika ambayo yalishirikisha utawala na watumishi wa maeneo husika. Katika mafunzo hayo watumishi hao walifundishwa jinsi ya kutumia Kompyuta na matumizi ya mfumo huo.

Aidha Bwana Katonyela amebainisha kuwa mafunzo mengine yataendelea kufanyika kati ya mwezi wa sita na saba mwaka huu.Mafunzo hayo yatalenga zaidi kuwajengea uwezo watumishi katika kuwa na mtazamo wa mabadiliko “Change management” ili iwe chachu ya kutumia vizuri mfumo huo pindi utakapoanza kufanya kazi.Lakini pia wahusika katika idara hizo husika watafundishwa jinsi mfumo huo wa Kompyuta unavyoweza kuleta mabadiliko katika utoaji Huduma.

Kwa hatua za awali hospitali hiyo inayotoa Huduma za rufaa imeonekana kukubali mabadiliko na imekuwa na matarajio makubwa kuhusu mfumo huo. Faida za kutumia mfumo huo wa Kompyuta “AfyaPro”  ni; kurahisisha kazi kwa  kukusanya  taarifa zilizo sahihi, kutoa ripoti kwa muda mfupi, kuongeza mapato na kupunguza foleni ambapo mgonjwa anahudumiwa haraka.

Mfumo huu unafadhiliwa na Taasisi ya  Kimataifa ya Mawasiliano na Maendeleo (IICD) ya nchini Uholanzi na unatumika kwenye baadhi ya hospitali zinazomilikiwa na Taasisi za dini na Serikali katika kanda ya ziwa. Hospitali hizo ni pamoja na Hospitali ya Nyamagana, Bukumbi na Magu, vituo vya afya Makongoro, Nyakato na zahanati za Nyakahoja, Imani Mwanza na Nasa. Mfumo huu wa Afyapro, unatumika kwenye baadhi ya vitengo kama vile; Mapokezi, Maabara, Stoo za madawa, wodi za wazazi na ofisi ya Mganga mkuu.Tume ya Kikristo ya Huduma za jamii (CSSC) inaratibu katika kusimamia mradi huo.

Views: 374

Add a Comment

You need to be a member of AfyaMtandao to add comments!

Join AfyaMtandao

© 2024   Created by sona.   Powered by

Badges  |  Report an Issue  |  Terms of Service