AfyaMtandao

Umoja ni dawa katika kukabiliana changamoto katika sekta ya afya na elimu –Peter Maduki

Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kikristo ya Huduma za jamii (CSSC), Bw. Peter Maduki ametoa wito kwa wamiliki na watendaji wa Taasisi za afya na elimu zinazomilikiwa na Makanisa kanda ya kaskazini kufanya kazi kwa ushirikiano na kuwa na umoja katika kusimamia Huduma hizo ambazo  zinatekelezwa na CSSC.

Bw. Maduki amesema hayo wakati akizungumza katika mkutano mkuu wa CSSC Kanda ya Kaskazini (Zonal Policy Forum) unaofanyika mjini Moshi

Amesema kuwa katika kufanikisha na kuboresha Huduma hizo lazima kuwe na mazingira mazuri ya ushirikiano baina ya watendaji wa Huduma hizo na wadau wengine kuanzia ngazi ya kituo husika hadi wilaya ili kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazokabili sekta hizo.

Aidha Bw. Maduki ametaja baadhi ya changamoto hizo kuwa ni suala la rasilimali watu na fedha ambalo bado ni tatizo katika sekta hizo, hivyo nguvu ya pamoja inahitajika katika kufanikisha malengo waliyojiwekea ya kuboresha zaidi Huduma hizo kwa kuzifanya kuwa bora zaidi.

Amewaomba wahusika kuweka mikakati ya kushirikishana kazi nzuri zinazofanywa na taasisi zao ili wengine waweze kujifunza kutoka katika taasisi zinazofanya vizuri. Ametoa mfano wa Huduma ya TibaMtandao ambayo inafanywa na baadhi ya hospitali kuwa ni nzuri na kuomba  hospitali zingine zihusishwe katika programu hiyo.

Pia Bw. Maduki ameelezea mipango ya baadaye ya CSSC kuwa ni pamoja na kuboresha kitengo cha utetezi (Lobbying), kuweka mkazo katika matumizi ya Teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA), kuboresha mfumo wa kuhifadhi taarifa za taasisi, uwezo na watumishi wake (Database) na  kuwaendeleza kielimu watumishi wa taasisi hizo ambao ni wanachama wake.

Akifungua Mkutano huo Mwenyekiti wa (ZPF) Kanda ya Kaskazini Askofu Paul Akyoo kupitia hotuba ilisomwa kwa niaba yake na Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kaskazini Dkt. Martin Shao, amesema mchango wa CSSC katika kuboresha Huduma za afya na elimu ni mkubwa, hivyo ni jukumu la kila mmoja kutekeleza wajibu wa kusimamia Huduma hizo.

Amesema kuwa CSSC Kanda ya Kaskazini iko katika mchakato wa kujenga ofisi yake ya kanda ambayo itarahisha zaidi Huduma za kiutendaji. Amebainisha kuwa eneo la ujenzi wa ofisi hiyo limepatikana na upembuzi yakinifu tayari umeishafanyika.

Mkutano wa ZPF Kanda ya Kaskazini unashirikisha Maaskofu wote wa Majimbo ya Kanisa Katoliki na Jumuiya ya Kikristo Tanzania wa mikoa ya Kanda hiyo ambayo ni Arusha, Manyara na Kilimanjaro na huwa unafanyika mara moja kwa mwaka.

 

Views: 344

Add a Comment

You need to be a member of AfyaMtandao to add comments!

Join AfyaMtandao

© 2024   Created by sona.   Powered by

Badges  |  Report an Issue  |  Terms of Service