Tume ya Kikristo ya Huduma za Jamii (CSSC), imejenga jengo la upasuaji, uzio wa kuzunguka hospitali, sehemu ya kufulia na kuanikia nguo, Maliwato na kuweka mashine ya kuteketezea takataka katika hospitali ya St. Francis iliyopo katika kijiji cha Kwamkono, tarafa ya Sindeni inayomilikiwa na Kanisa la Anglicana, wilayani Handeni mkoani Tanga, vyote vikiwa na thamani ya Sh. 995 millioni.
Mbali na ujenzi huo ambao umefanyika kwa ufadhili wa Serikali ya Ujerumani kupitia Benki ya Maendeleo ya Ujerumani (KfW), pia hospitali hiyo imekabidhiwa vifaa mbalimbali vya upasuaji.
Akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi jengo hilo wilayani Handeni, Naibu Waziri wa Afya na ustawi wa Jamii, Dkt. Seif Rashid, aliipongeza serikali ya Ujerumani iliyofadhili ujenzi huo, KfW na wasimamizi wa mradi huo CSSC.
Dkt. Seif alibainisha kuwa huo ni mchango mkubwa katika kuboresha upatikanaji wa Huduma za afya hapa nchini, tofauti na misaada mingine, akionyesha kuwa mchango, huo umelenga kuboresha maisha ya Watanzania, kwani bila huduma bora za afya na elimu hakuna maendeleo ya kweli.
Aidha Dkt. Seif ameelezea kuwa Serikali imeendelea kudumisha ushirikiano na sekta binafsi yakiwemo mashirikaya dini ili kuwezesha sekta hizo kuwa na mazingira yanayoiwezesha ukamilifu katika utoaji wa Huduma za afya.
Meneja Mradi kutoka CSSC, Grace Mwang’onda, anasema ujenzi wa jengo hilo ni sehemu ya mradi mkubwa wa kusaidia sekta ya afya ambao unafadhiliwa na Serikali ya Ujerumani,na mradi huo ulianza kutekelezwa mwaka 2009 na kukamilika mwezi Desemba, 2013. Anatoa rai kwa wahusika kulitunza Jengo hilo ili liendelee kubaki katika hadhi yake.
Bunge wa jimbo la Handeni, Dkt . Abdallah Kigoda, alisema wilaya hiyo ina asilimia 33 ya wakazi wote wa Tanga; hivyo hospitali hiyo ni muhimu ikaboreshwa kwani inategemewa na wananchi wengi.Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Muhingo Rweyemamu, alipongeza wafadhili kwa kufanikisha jengo hilo la upasuaji na kuongeza kuwa uongozi wa mkoa unaipa nafasi kubwa hospitali hiyo.
Naye Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Dkt. George Chausa, alisema hospitali hiyo ambayo ilianzishwa mwaka 1917 inakabiliwa na uchakavu wa majengo na upungufu wa vifaa tiba. Alisema hospitali hiyo ni miongoni mwa hospitali mbili ambazo zinategemewa na wananchi wa wilaya hiyo.
© 2024 Created by sona. Powered by
You need to be a member of AfyaMtandao to add comments!
Join AfyaMtandao