AfyaMtandao

TCMA yaadhimisha Jubilee ya miaka 75

CHAMA cha Madaktari wa Kikristo Tanzania (TCMA), kimeeleza kuwa asilimia kubwa ya vituo vya afya vilivyopo maeneo ya vijijini vinakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo uhaba wa rasilimali watu jambo ambalo linakwamisha maendeleo ya afya vijijini.Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa TCMA, Dk. Isaya Tosiri, wakati wa kongamano la  Jubilee ya miaka 75 ya chama hicho tangu kuanzishwa kwake mwaka 1937, ambapo mgeni rasmi katika ufunguzi huo alikuwa Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii Bi. Regina Kikuli.

 

Dk. Tosiri amesema kuwa suala la rasilimali watu limekuwa ni tatizo kubwa katika vituo vya afya hivyo hali inayopelekea utendaji wa kazi kuwa mgumu. Ametoa wito kwa Serikali kuangalia namna ya kusaidia upatikanaji wa wataalum wenye sifa na vifaa tiba ili kuendelea kutoa huduma bora zaidi, sambamba na kuboresha mazingira ya kazi kwa watumishi.

 

Aidha Dk. Tosiri amebainisha kuwa suala la mishahara na malupulupu kwa madaktari limekuwa na changamoto kubwa hali inayofanya madaktari wengi kukimbia kutofanya kazi katika maeneo ya vijijini.

 

Dk. Tosiri amefafanua kuwa, pamoja na changamoto hizo bado chama chake kwa kushirikiana na Taasisi husika wamejitahidi kupambana katika kuzitafutia ufumbuzi changamoto hizo.

 

Kwa upande wake Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii Regina Kikuli alisema serikali imejipanga kukabiliana na tatizo la uhaba wa railimali watu kwa kwa kuongeza udahili kwa wanafunzi wa taaluma ya udaktari kutoka 1013 hadi 7000 kwa vyuo vyote nchini.

 

Alisema ongezeko hilo la udahili ni moja ya njia ya kukabiliana na uhaba wa rasilimali watu  katika sekta ya Afya nchini.Bi. Kikuli amekiri kuwa suala la ongezo la mishahara ya madaktari ni la msingi lakini bado nalo lina changamoto kubwa ambayo serikali inalitazama kwa mapana yake na kulitafutia ufumbuzi wa kudumu.

 

“Ni kweli madaktari wanakabiliwa na changamoto nyingi lakini serikali pia imeamua kushirikiana kikamilifu na taasisi hizo ili kutatua kero hizo na kuweka mazingira mazuri  na salama ya kazi. Alisema Bi. Kikuli

Alisema serikali kwa sasa inampango wa kujenga nyumba za madaktari vijijini ikiwa ni moja ya mikakati ya kuboresha mazingira ya kazi.

 

Maadhimisho ya Jubilee ya miaka 75 ya Chama cha Madaktari wa Kikristo Tanzania (TCMA) yalifanyika Katika Ukumbi wa Baraza la maaskofu Tanzania (TEC) na kuhudhuriwa na washiriki ambao ni watumishi wa afya zaidi ya 300 kutoka katika vituo mbalimbali vya afya vinavyomilikiwa na madhehebu ya Kikristo.

Views: 481

Add a Comment

You need to be a member of AfyaMtandao to add comments!

Join AfyaMtandao

© 2024   Created by sona.   Powered by

Badges  |  Report an Issue  |  Terms of Service